Elimu butu Haitatufikisha popote
Taifa lolote linalonia makubwa; Taifa lenye njozi za masafa marefu. Taifa lenye maono na, linalokusudia kufikishwa mbali kupitia maono hayo linapaswa, kabla ya yote, kuwekeza kwenye elimu bora. Elimu yenye kuaksi mahitaji na vipaumbele vya taifa husika. Elimu ambayo mtaala wake ni matokeo ya utafiti wa kutosha uliojikita katika kujaribu kutengeneza jamii ya watu wanaojitambua, kujithamini na kujikubali huku ikitambua fursa zilizopo. Jamii inayotambua kule ilikotoka pale ilipo na kule iendako.
Elimu ya aina hii aghalabu haipimwi kwa vigezo vya gredi, au tuseme vidato na michuano ya ufahamu wa nadharia bali hupimwa kwa kuzingatia mshehenezo wa utajiri wa maarifa kama mtaji wenye kuweza kutumika kikamilifu ndani ya mduara wa fursa adhimu na hazina ghafi zilizopo kwa manufaa ya jamii husika.
Ili kufanikisha hili, suala la gharama na utendaji wa kimazingaombwe huwekwa pembeni, kipaumbele huwa ni kuwekeza katika ubongo, maarifa, Naam, stadi stahiki kwa gharama yoyote ile ili kutengeneza krimu ya wasomi bora ambao hatimaye huleta mrejesho wa tunu maridhawa. Tunu inayorudisha mwangwi mwororo unaoiburudisha na kuinufaisha jamii yote sawia!
Jamii inayonyanyapaa uwekezaji katika Elimu na wakati huo-huo ikitegemea kupata mavuno ya raia bora na wenye sifa stahiki hiyo ni jamii iliyopea kwenye tasnia ya ushirikina wa kufikiri nje ya muktadha halisia. Jamii ya namna hii haiogopi kufanya mazingaombwe ya kugeuza mawe ili yawe mkate ili tu kukidhi haiba fifi ya akili bweteko. Akili iliyovia na kupungua kinga-ubongo dhidi ya magojwa nyemelezi ya ujuha wa ki-mfumo utokanao na athari za virusi vya Elimu butu ya kukopi na kubandika, kwa kimombo chenye mchanyato wa kiswahili ku-copy na ku- pest!
Na hata kindumbwendumbwe cha matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Naam, matokeo yaliyopelekea kufinyangwa kwa tume ya chapuchapu iliyokuja na majibu ya chapuchapu kwa maswali magumu; na hatimaye kufuta matokeo kwa stahili ya danganya toto ili kuibuka na matokeo yenye upya feki; kwa maana ya mvinyo uleule wa kale, lakini ndani ya viriba vipya, ni, sehemu ya mwendelezo wa jamii yenye Elimu ya kimazingaombwe. Jamii iliyokubuhu kwa kujidanganya. Jamii ya watu wanaonawili sura zao pale wanapopigiwa makofi na wingu la mashahidi waliokolea kilevi cha Elimu butu isiyoweza kuwapa maarifa ya kupembua baina ya chuya na mchele.
Jamii ya namna hii huzaa viongozi wasioogopa kufinyanga matokeo. Viongozi wenye uso mgumu. Uso wa gumegume usioona soni kufanya matendo ya miujiza feki kwenye ukanda nyeti wa Elimu. Miujiza inayoweza kulinganishwa na uchuro wa kukatisha kwenye mitaa iliyofurika utitiri wa watu kwa mbwembwe, kwa imani kuwa mungu wao kawavika joho memetufu la dhahabu tupu, joho lenye kuonwa na watakatifu tu; hata kama kuna kundi la watu wachache wenye jicho la tatu, wanaotoa mvumo tulivu wa hekima ya kuwa “mfalme yuko uchi, na avikwe nguo!”
Viongozi waliotengenezwa na mfumo wa Elimu ya namna hii hupendezwa sana na ujumbe wa manabii feki wenyewe kalamu hodari za kuwasifia na kuwatabiria mambo mema hata kama mambo yanakwenda ndivyo sivyo. Nguvu zao kubwa huwekeza katika kutafuta njia za mkato-mkato na kutafuta majibu mapesi-mepesi kwa maswali magumu, yanayohitaji uwekevu wa akili jadidi inayokwenda kwa mikito sahihi ya kimaamuzi.
Tukumbushane.Nilipoandika kupinga, suala la mtu mmoja kujiuzulu kutokana na madudu yanayoendelea ndani ya viunga vya Elimu ya Tanzania, wengi walinitafsiri ndivyo sivyo, wakidhani ya kuwa kalamu yangu inadondosha wino kwa lengo la kutengeneza kinga, kwamba waziri wa Elimu asiadhibiwe.
Lakini ukweli ni huu; darubini yangu ya kimaono ilinipa, na bado ingali inanipa, taswira ya kwamba tatizo la Elimu nchini Tanzani ni la kimfumo zaidi. Tatizo ambalo, msemo wa Bwana Yesu, hata akitumwa mtu toka kwa wafu hatoweza kuleta jambo jipya. Niongezee; Hata kama tungempata Waziri wa Elimu mwenye upeo wa malaika aliyesheheni akili zisomfano atabakia na ubunifu wake mwenyewe kichwani. Ndio maana tunaendelea kuibuka na mawazo ya ajabu-ajabu la kukopi na kupesti, eti, mtoto wa miaka mitatu iwe lazima kwenda shule. Kwa stahili hii ni lini mtoto huyu atapata mkumbatio wa kisaikolojia wa mama? Wataalam wetu wa wa saikolojia ya Elimu wako wapi kupinga fikra hizi butu?
Kwa nini tudandie mfumo wa Elimu wa ma-globalisti wenye ajenda fifi ya kuharibu kizazi chetu kupitia Elimu ya ki-globalisti inayodhoofisha Elimu ya kifamilia ambayo ni muhimu kwa jamii yoyote lenye kupania kuwa na taifa la watu wenye maadili? Kama Waziri Membe amegundua kuwa ICC ni kwa ajili ya kusukuma ajenda za kibeberu, ni vema akatambua kuwa hata mfumo huu mpya wa Elimu uliobuniwa na mainjinia wa serikali moja ya dunia ni mwendelezo uleule wa kuwaburuza waafrika! Nakazia kwamba; Tiba ya kimfumo haiwezi kupatikana kwa kunyofoa tofari moja-moja, bali ni kuusambaratisha mfumo, tuseme, jengo husika na kuja na mfumo mpya wenye kukidhi viwango stahiki.
Nikirejea kwenye hoja yetu, kwa mtazamo wangu, suala la kupandisha kiwango cha ufaulu lililobuniwa na mgwiji wetu wa Elimu lilikuwa ni jambo muhimu sana. Huo ulikuwa ni mwanzo mpya wa ufumuaji wa mfumo butu wa Elimu. Wangelikaza kamba bila kurudi nyuma, kwani hiyo ilikuwa ni hatua mzuri katika mapinduzi ya Elimu. Inasikitisha kwamba, waliposikia kelele za vyura kwenye dimbwi wamerudi nyuma wasijatuliza kiu ya kweli!
Hawakurudi tu nyuma; kubwa zaidi linaloniogofya ni uamuzi huu mpya wa kufinyanga matokeo kwa lengo la kunyamazisha mvumo na kelele za kimakengeza toka kwa jamii iliyotwama ndani ya dimbwi la kipropaganda . Je, kwa uamuzi wa kufinyanga matokeo tunatibu au tunabomoa? Na, Je, ina maana magwiji wetu walioketi pamoja na hatimaye kufanya maamuzi haya mazito walikuwa wamekunywa mvinyo mpya? Au tuamini, msemo wa mheshimiwa ndugai walipuliza ile sigara kubwa? Tutulize vichwa vyetu ili kutafakari!
Kwa tafakuri yangu naamini kwamba baraza la mitihani kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu walikuwa sahihi kabisa kuweka vigezo vya ufaulu ambavyo angalau vinakubalika kimataifa. Na kwamba hata kungekuwa na miaka mia moja ya kuwaandaa walimu na wanafunzi, kama wengi wanavyojenga dai lao, ili kufikia vigezo hivyo tusingeweza kuvifikia bila kuwa na mikakati yakinifu inayokwenda sambamba na uwekezaji wa kutosha. Kutovifikia vigezo hivyo hakuondoi sifa za ubora wa uamuzi huo muhimu,
Lakini kuendelea na vigeza hafifu vyenye kukidhi mahitaji ya chapuchapu, ya kuwavutia vipofu, ni kuogelea ndani ya madudu ya kimfumo. Tusingerudi nyuma; tungesonga mbele huku tukilifanyia kazi wazo nyeti la mbunge wa kuteuliwa James Mbatia ya kwamba hadi sasa hatuna mtaala unaoeleweka, hivyo hatuna budi kuwa na mtaala wa Elimu ulio makini wenye kuzingati mahitaji na vipaumbele vya taifa vya sasa na vya siku za usoni. Hata hivyo hatua hiyo isingetuondoa kwenye ukweli mtukuka ya kwamba mtaala uliokosa watu mahili wa kuutendea kazi ni sawa na shamba bora lililokosa mkulima, au mtu mwenye upara mng’aavu lakini mtindivu wa hekima na busara.
Kwa mtazamo ulio yakinifu, hata suala la kuandaa mtaala ni suala la kimchakato linalohitaji utafiti na upembuzi yakinifu. Si jambo la mwaka mmoja, miaka miwili au mitatu maana Mtaala ni sawa na dira na maono ya Taifa. Hatuwezi kuandaa mtaala bora kwa staili ya kidharura-dharura. Tunahitaji utafiti mtwamivu chini ya watafiti watwamivu, tena, wenye uzalendo mtwamivu!
Hapa tulipo wasomi wetu hawajaandaliwa kumiliki gesi mafuta uramu na utitiri mwingi wa rasilimali. Tunaparurana kwa harufu tu ya samaki. Hatujaona mnofu. Wasomi wetu hawajaandaliwa kupambana na ubeberu wa kimfumo katika mkutadha wa kimataifa, mfano ICC Kama taifa Hatujui kuwa tunaongozwa na itikadi gani; ya kijamaa au ya kibepari. Ni kizungumkuti! Ni mtikisiko wa kimaono. Kama tutasema tunajua tulikotoka na tulipo, lakini ni hakika hatujui tuendako. Msemo wa hayati Kolimba kama Taifa tumekosa dira. Abusolomo Kibanda anadakia akisema huko tuendako kweli tutafika? Ni mtaala ndio unaoweza kujibu haya yote.
Kwa maana nyingine kitendo cha kufuta matokeo ili kujipatia matoke mapya ya kupikwa ni sawa na kula chungwa lililooza ndani ya chumba kilichogubikwa na giza totoro huku tukijifariji kuwa, kwa vile hatuwaoni funza basi machungwa hayo hayana mathari kwetu. Hapa kama taifa, hatujajitendea haki hata kidogo. Tumejikaanga kwa mafuta yetu wenyewe!
Joshua Lawrence 0717047907
RAIS OBAMA: NA PROPAGANDA ZA KUTAWALA FIKRA ZA WASOMI WA KIAFRIKA
Uko mkakati mzito unaoendelea chini kwa chini ili kuhakikisha kuwa dunia yote inatweka vilindini mwa mfumo wa kimaadili unaopwaya siku si mbali tokea sasa. Kwa hakika huo ni mkakati yakinifu unaoratibiwa kwa weledi mkubwa huku watu wenye misuli ya kimaamuzi wakishikilia mwelekeo mzima wa ajenda hii tete na tata; Tutaangalia.
Wakati msukumo huo ukiendelea kutengeneza mwelekeo wa kimaadili ulio legelege, huku wale wote wanaojitahidi kusimama katika misingi kimaadili wakiwekwa fungu moja na kundi ya wahafidhina, watu waliathiriwa na misimamo ya kidogima isiyofungua wigo kwa mawazo mapya, kuna kila dalili zinazoonesha kuwa hatimaye dunia nzima, isipokuwa kundi la watu wachache, itapigishwa magoti chini ya bendera ya mfumo wa kimaadili mdhofu utakaokuwa kama jeneza la mataifa tayari kwa mazishi.
Hatari iliyo kubwa zaidi, ni pale hoja hizi momonyovu kimaadili zinapopenyezwa taratibu ndani ya mifumo ya kisheria huku zikiwa zimevikwa magwandwa yenye rangi ya kidemokrasia na usawa kwa wote na hivyo kulichora kundi kinzani katika taswira fifi iliosheheni makengeza ya hitifaki ya usasa, unaoenzi misingi ya usawa na utu!
Mkakati huo unakwenda sambamba na upropagandisha uliokubuhu kwa hila, ili kutengeneza taswira isiyo sahihi kuhusu muktadha jumla wa dhana nzima ya neno maendeleo. Kwamba, wakati muktadha uhusuo dhana ya maendeleo ya kweli wapaswa kumulikwa katika nyanja zote kwa ukamilifu wake, yaani; kiakili, kiafya, kimaadili na matumizi sahihi ya raslimali ndani ya kijamii husika, mataifa ya magharibi yanajaribu kujikita zaidi katika mtazamo finyu wa utajiri wa vitu; nyumba, magari, na vikorombwezo vyake, huku maeneo mengine muhimu hata kuzidi vikorombwezo hivyo yakiacha pembeni.
Katika harakati zao za kuudororesha mfumo wa kimaadili, tarehe 17 Juni mwaka 2011 dunia yote ilishuhudi Umoja wa Mataifa ukipitisha ajenda ya kuhalalisha ndoa ya jinsia moja. Tamko hilo lenye ukakasi kimaadili, ambalo kwa lugha sahihi nituseme ni azimio la umoja wa Mataifa, lilisomwa na aliyekuwa katibu wa Rais Barack Obama bibi Hilary Clinton. Afrika Kusini ndio Waliokuwa wafadhili wakuu wa michakato yote hadi hitimisho lake.
Baada tu ya tamko hilo, ulimwengu umeshuhudia anguko la ghafla kimaadili huku matamko toka vinywa vizito yakijitahidi kuinawilisha ajenda hii kwa lengo la kuijengea misuli ya kimvuto ndani ya katiba za nchi mbalimbali duniani. Mataifa yaliyoongeza msululu ndani ya safari ya mporomoko kimaadili ni kama vile Uingereza, Ufaransa, na mengine yako mbioni kufuata foreni hii, inayoongozwa na mkuu wa giza!
Katika hili, Umoja wa Mataifa chini ya Katibu Mkuu wa sasa, mheshimiwa Ban ki Moon, umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa viongozi wa juu wa mataifa yote wanasimamia kwa umakini mkubwa utekelezaji wa azimio hili; Tanzania ni moja ya nchi wahanga wa msukumo huo wenye ladha ya kisodoma na Gomora!
Ukiwa kama mwendelezo wa ajenda hii, hivi karibuni katika ziara yake barani Afrika, akiwa nchi Senegal, Barack Obama, ametoa hotuba mbele ya Rais wa nchi hiyo akihimiza kuwa yeye kama muumini wa usawa, angependa kuona kuwa mashoga wanapewa haki yao kisheria pasipo kubaguliwa. Hata hivyo kauli hiyo ilijibiwa hapo-hapo na Rais huyo jasiri akisema kuwa katu taifa lake haliwezi kusigana na maadili ya kitaifa kwa kuhalalisha ushenzi huo.
Hata hivyo jibu hilo lenye mshehenezo wa hekima ya kimbingu halikumfanya rais Obama kuendelea na kile ambacho kwa hakika kingeweza kutafsirika kama mashindano, ndani ya mdahalo usio rasmi, zaidi ya kumalizia kwa kusema kuwa yeye kama Rais wa Marekani mwenye kuamini juu ya usawa, hayupo pale kwa lengo la majadiliano.
Wadadavuzi wabobevu wa siasa za dunia, wanaamini kuwa kauli ya Obama yaweza kubeba uzito mkubwa kuliko ambao bongo zenye kunyanyapaa usumbufu wa kufikiri zinavyoweza kuipa. Na, kwamba hakuna taifa lenye utapiamlo kimaadili liwezalo kusonga mbele kiuchumi. Historia imehifadhi kwa uaminifu kumbukumbu ya anguko la mataifa makubwa yaliyowahi kutikisa dunia ikiwemo dola ya Rumi, ya kwamba sababu ya anguko la mataifa haya yote ilitokana na kutindikiwa kimaadili kulikoyafanya yashindwe kujisimamia yenyewe.
Kwa mwanga ulio bora zaidi, Obama hafanyi ziara Afrika kwa lengo ya kutafuta, tuseme, mwafaka wenye kutegemezwa na uhuru wa waafrika kujiamulia masuala yao ndani ya mataifa yao, bali ni sehemu ya mwendelezo wa mradi mpevu wa kuhandisi bongo za wasomi wetu katika mwelekeo utakaokuwa na tija kwa taifa la Marekani na wapambe wake, huku miundombinu ya kimaadili ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli ikiporomoshwa chini kupitia propaganda fifi zenye ladha feki ya upanuzi wa demokrasia.
Hata kongamano lililobeba jina tukufu “Global Smart Partnerships” si wazo handisivu kupitia vinu vya bongo za waafrika, bali ni mwendelezo wa propaganda za kimagharibi zenye lengo la kuwapumbaza waafrika, ili waendelee kupigana na adui feki kiuchumi, ambaye kwa hakika siyo mvio wa mataifa ya Afrika kiteknolojia, bali ni mvio wa bongo za wasomi wetu, na tiba ya kweli yapaswa kujikita hapo.
Kwa hakika, jitihada zozote zisizojikita katika ujenzi wa miundombinu ya kimaadili na kimenejimenti ndani ya mkutadha wa ombwe la usimamizi makini wa rasilimali vitu na watu, hugeuka sehemu ya mwendelezo wa usambaratishaji wa maadili, kwa maana ya kutoruhusu uwekevu wa mawazo mapevu juu ya adui wa kweli wa mataifa ya kiafrika, ambaye ni udhaifu wa kusimamia raslimali zilizopo, zikiwemo raslimali watu kwa ajili ya manufaa ya waafrika.
Udhaifu huo ndiyo uliofanikisha uundwaji wa dola za kifisadi zenye kutengeneza minyororo yenye miale mikali itiayo kiwi mboni za wahandisi wenye uzalendo na bara hili ikiwemo Tanzania. Kwa mfano; ni nani asiyejua kwamba Symbion ni mjukuu wa Richmond aliyetuzalia watanzania mwana wa pekee kwa nina aitwaye Downs.
Je, intelijensia ya Barack Obama haijampa taarifa juu ya sakata hili. Ya kuwa joka linalokunya maziwa ya watanzania linafugwa na Amerika? Kama kweli Obama ana nia ya dhati ya kuwakomboa waafrika, na, anatutakia watanzania jioni njema yenye mafanikio kiuchumi; Kwanini atumie wakati wake wa thamani kubariki ufisadi uliopo pale Ubungo badala ya kuusambaratisha kupitia mjadara wa kimataifa kama huo?
Kuhusu mada inayojenga dailojia ya “Global Smart Partnerships; Je, ni kweli kwamba tunahitaji teknolojia ya hali ya juu ili tuvuke hapa tulipo kiuchumi? Je, ili kubaini ukweli ya kwamba, wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya madini, wakiwemo wamarekani wenyewe hawalipi kodi na hivyo kulidumaza taifa kiuchumi kwa kulikosesha mapato ambayo ni muhimu kwa maendeleo kiuchumi, kweli tunahitaji teknolojia?
Je, tunahitaji teknolojia ili kubaini wizi wa mamilioni ya tani za minofu ya samaki yanayosafirishwa kwa meli kila siku kwenda china na penginepo? Nauliza watanzania wenzangu, naomba majibu stahiki! Je, ili kutambua kuwa utajiri wa uramu na gesi tulio nao waweza kututoa kutoka kwenye lindi la umaskini hadi kuwa vileleni mwa mataifa tajiri iwapo tutatanguliza uzalendo tunahitaji teknolojia gani?
Je, tunahitaji teknolojia ili kuzuia utoroshaji wa wanyama, na uvunaji wa magogo huku udongo wenye madini na vito vikisafirishwa kwenda ughaibuni kwa gia iliyojaa ghiliba?
Si kwamba napingana na uwekezaji kwenye Elimu ya teknoloji, bali siamini kwa Afrika iko nyuma kimaendeleo kwa sababu iko nyuma kiteknolojia. Hizo ni propaganda za mataifa ya magharibi Hoja mtambuka ni kwamba; kwa kusimamia raslimali zetu kwa uadilifu huku tukitangukliza uzalendo tungefika mbali sana kiuchumi. Kuna mifano ya nchi za kiarabu ambazo kwa usimamizi wa mafuta tu, hivi sasa ni tajiri, mfano Botswana, kwa kusimamia vizuri madini ya dhahabu hali za wananchi wake ni bora.
Mjadala wa Global Smart Partnerships ungetutendea haki waafrika kama ungelenga katika kupambana na mfumo kandamizi wa mataifa makubwa kupitia World Bank na IMF. Mjadala huo ingeleta tija kiuchumi kama ungelenga katika kuyabana makampuni ya kigeni yanayokwepa kodi na uwekezaji katika ardhi ya waafrika uliokosa rojo ya urari. Naam, mjadala huo ungejielekeza katika kuwabana watawala, na sio viongozi, wa kiafrika wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kukandamiza demokrasia yenye mshehenezo wa maadili safi yanayokinzana na demokrasi ya kuruhusu ushoga.
Bara la Afrika haliwezi kutegemea ukombozi wa kweli kiuchumi kupitia mawazo na makongamano yaliyohandisiwa kwa weledi mkubwa na mataifa ya magharibi. Huko ni kujidanganya, kwani roho ya kutawala fikra za waafrika iliyowatafuna mababu zetu nyakati za ukoloni mkongwe ni ileile inayojipambambanua katika sura ya utandawazi.
Kwa jinsi mwelekeo wa mambo ulivyo ni vema nikahitimisha makala hii kwa kutamka bayana kuwa, ili kujikomboa kiuchumi, Afrika inahitaji Afrika Smart Partnerships na siyo Global Smart Partnerships.
Kuendelea kukumbatia fikra za kizungu kama nyenzo ya kututoa hapa tulipo, hakutofautiani kabisa na ukahaba wa akili unaokwenda sambamba na ukuadishaji wa bongo za kisomi ndani ya mzunguko usio na mwisho wa fikra mfilisi zinazotegemezwa na mirindimo ya fikra twezo za kimagharibi. Tafakari kasha chukua hatua!
drjoshualawrence@yahoo.com au 0753333003







0 comments:
Post a Comment