Elimu butu Haitatufikisha popote

Thursday, July 4, 2013



Taifa lolote linalonia makubwa; Taifa lenye njozi za masafa marefu. Taifa lenye maono na, linalokusudia kufikishwa mbali kupitia maono hayo linapaswa, kabla ya yote, kuwekeza kwenye elimu bora. Elimu yenye kuaksi mahitaji na vipaumbele vya taifa husika. Elimu ambayo mtaala wake ni matokeo ya utafiti wa kutosha uliojikita katika kujaribu kutengeneza jamii ya watu wanaojitambua, kujithamini na kujikubali huku ikitambua fursa zilizopo. Jamii inayotambua kule ilikotoka pale ilipo na kule iendako.

Elimu  ya aina hii aghalabu haipimwi kwa vigezo vya gredi, au tuseme vidato na michuano ya ufahamu wa nadharia bali  hupimwa kwa kuzingatia mshehenezo wa utajiri wa maarifa kama mtaji wenye kuweza kutumika kikamilifu ndani ya mduara wa fursa adhimu na hazina ghafi zilizopo kwa manufaa ya jamii husika.

Ili kufanikisha hili, suala la gharama na utendaji wa kimazingaombwe huwekwa pembeni, kipaumbele huwa ni kuwekeza katika ubongo, maarifa, Naam, stadi stahiki  kwa gharama yoyote ile ili kutengeneza krimu ya wasomi bora ambao hatimaye huleta mrejesho wa tunu maridhawa.  Tunu inayorudisha mwangwi mwororo unaoiburudisha na kuinufaisha jamii yote sawia!



Jamii inayonyanyapaa uwekezaji katika Elimu na wakati huo-huo ikitegemea kupata mavuno ya raia bora na wenye sifa stahiki  hiyo ni jamii iliyopea kwenye tasnia ya ushirikina wa kufikiri nje ya muktadha halisia. Jamii ya namna hii haiogopi kufanya mazingaombwe ya kugeuza mawe ili yawe mkate ili tu kukidhi haiba fifi ya akili bweteko. Akili iliyovia na kupungua kinga-ubongo dhidi ya magojwa nyemelezi ya ujuha wa ki-mfumo utokanao  na athari za virusi vya Elimu butu ya kukopi na kubandika, kwa kimombo chenye mchanyato wa kiswahili ku-copy na ku- pest!

Na hata kindumbwendumbwe cha matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Naam, matokeo yaliyopelekea kufinyangwa kwa tume ya chapuchapu iliyokuja na majibu ya chapuchapu kwa maswali magumu; na hatimaye  kufuta matokeo kwa stahili ya danganya toto ili kuibuka na matokeo  yenye upya feki;  kwa maana ya mvinyo uleule wa kale, lakini ndani ya viriba vipya, ni, sehemu ya mwendelezo wa jamii yenye Elimu ya kimazingaombwe. Jamii iliyokubuhu kwa kujidanganya. Jamii ya watu wanaonawili sura zao  pale wanapopigiwa makofi na wingu la mashahidi waliokolea kilevi cha Elimu butu isiyoweza kuwapa maarifa ya kupembua baina ya chuya na mchele.

Jamii ya namna hii huzaa viongozi wasioogopa kufinyanga matokeo. Viongozi wenye uso mgumu. Uso wa gumegume usioona soni kufanya matendo ya miujiza feki kwenye ukanda nyeti wa Elimu. Miujiza inayoweza kulinganishwa na uchuro wa  kukatisha kwenye mitaa iliyofurika utitiri wa watu  kwa mbwembwe, kwa imani kuwa mungu wao kawavika joho memetufu la dhahabu tupu, joho lenye kuonwa na watakatifu tu; hata kama kuna kundi la watu wachache wenye jicho la tatu, wanaotoa mvumo tulivu wa  hekima ya kuwa “mfalme yuko uchi,  na avikwe nguo!”

Viongozi waliotengenezwa na mfumo wa Elimu ya namna hii hupendezwa sana na ujumbe wa manabii feki wenyewe kalamu hodari za kuwasifia na kuwatabiria mambo mema hata kama mambo yanakwenda ndivyo sivyo. Nguvu zao kubwa huwekeza katika kutafuta njia za mkato-mkato na kutafuta majibu mapesi-mepesi kwa maswali magumu, yanayohitaji uwekevu wa akili jadidi inayokwenda kwa mikito sahihi ya kimaamuzi.

Tukumbushane.Nilipoandika kupinga, suala la mtu mmoja kujiuzulu kutokana na madudu yanayoendelea ndani ya viunga vya Elimu ya Tanzania, wengi walinitafsiri ndivyo sivyo, wakidhani ya kuwa kalamu yangu inadondosha wino kwa lengo la kutengeneza kinga, kwamba waziri wa Elimu asiadhibiwe.

Lakini ukweli ni huu; darubini yangu ya kimaono ilinipa, na bado ingali inanipa, taswira ya kwamba tatizo la Elimu nchini Tanzani ni la kimfumo zaidi. Tatizo ambalo, msemo wa Bwana Yesu, hata akitumwa mtu toka kwa wafu hatoweza kuleta jambo jipya. Niongezee; Hata kama tungempata Waziri wa Elimu mwenye upeo wa malaika aliyesheheni akili zisomfano atabakia na ubunifu wake mwenyewe kichwani. Ndio maana tunaendelea kuibuka na mawazo ya ajabu-ajabu la kukopi na kupesti, eti, mtoto wa miaka mitatu iwe lazima kwenda shule. Kwa stahili hii ni lini mtoto huyu atapata mkumbatio wa kisaikolojia wa mama? Wataalam wetu wa wa saikolojia ya Elimu wako wapi kupinga fikra hizi butu?

Kwa nini tudandie mfumo wa Elimu wa ma-globalisti wenye ajenda fifi ya kuharibu kizazi chetu kupitia Elimu ya ki-globalisti inayodhoofisha Elimu ya kifamilia ambayo ni muhimu kwa jamii yoyote lenye kupania kuwa na taifa la watu wenye maadili? Kama Waziri Membe amegundua kuwa ICC ni kwa ajili ya kusukuma ajenda za kibeberu, ni vema akatambua kuwa hata mfumo huu mpya wa Elimu uliobuniwa na mainjinia wa serikali moja ya dunia ni mwendelezo uleule wa kuwaburuza waafrika! Nakazia kwamba; Tiba ya kimfumo haiwezi kupatikana kwa kunyofoa tofari moja-moja, bali ni kuusambaratisha mfumo, tuseme, jengo husika na kuja na mfumo mpya wenye kukidhi viwango stahiki.

 Nikirejea kwenye hoja yetu, kwa mtazamo wangu, suala la kupandisha kiwango cha ufaulu lililobuniwa na mgwiji wetu wa Elimu lilikuwa ni jambo muhimu sana. Huo ulikuwa ni mwanzo mpya wa ufumuaji wa mfumo butu wa Elimu. Wangelikaza kamba bila kurudi nyuma, kwani hiyo ilikuwa ni hatua mzuri katika mapinduzi ya Elimu. Inasikitisha kwamba, waliposikia kelele za vyura kwenye dimbwi wamerudi nyuma wasijatuliza kiu ya kweli!
                                                                                    
Hawakurudi tu nyuma; kubwa zaidi linaloniogofya ni  uamuzi huu mpya wa  kufinyanga matokeo kwa lengo la kunyamazisha mvumo na kelele za kimakengeza toka kwa jamii iliyotwama ndani ya dimbwi la kipropaganda . Je, kwa uamuzi wa kufinyanga matokeo tunatibu au tunabomoa? Na, Je, ina maana magwiji wetu walioketi pamoja na hatimaye kufanya maamuzi haya mazito walikuwa wamekunywa mvinyo mpya?  Au tuamini, msemo wa mheshimiwa ndugai walipuliza ile sigara kubwa? Tutulize vichwa vyetu ili kutafakari!

Kwa tafakuri yangu  naamini kwamba baraza la mitihani kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu walikuwa sahihi kabisa kuweka vigezo vya ufaulu ambavyo angalau vinakubalika kimataifa. Na kwamba hata kungekuwa na miaka mia moja ya kuwaandaa walimu na wanafunzi, kama wengi wanavyojenga dai lao, ili kufikia vigezo hivyo tusingeweza kuvifikia bila kuwa na mikakati yakinifu inayokwenda sambamba na uwekezaji wa kutosha. Kutovifikia vigezo hivyo hakuondoi sifa za ubora wa uamuzi huo muhimu,

 Lakini kuendelea na vigeza hafifu vyenye kukidhi mahitaji ya chapuchapu, ya kuwavutia vipofu, ni kuogelea ndani ya madudu ya kimfumo. Tusingerudi nyuma; tungesonga mbele huku tukilifanyia kazi wazo nyeti la mbunge wa kuteuliwa James Mbatia ya kwamba hadi sasa hatuna mtaala unaoeleweka, hivyo hatuna budi kuwa na mtaala wa Elimu ulio makini wenye kuzingati mahitaji na vipaumbele vya taifa vya sasa na vya siku za usoni. Hata hivyo hatua hiyo isingetuondoa kwenye ukweli mtukuka ya kwamba mtaala uliokosa watu mahili wa kuutendea kazi ni sawa na shamba bora lililokosa mkulima, au mtu mwenye upara mng’aavu lakini mtindivu wa hekima na busara.

Kwa mtazamo ulio yakinifu, hata suala la kuandaa mtaala ni suala la kimchakato linalohitaji utafiti na upembuzi yakinifu. Si jambo la mwaka mmoja, miaka miwili au mitatu maana Mtaala ni sawa na dira na maono ya Taifa. Hatuwezi kuandaa mtaala bora kwa staili ya kidharura-dharura. Tunahitaji utafiti mtwamivu chini ya watafiti watwamivu,  tena, wenye uzalendo mtwamivu!

Hapa tulipo wasomi wetu hawajaandaliwa kumiliki gesi mafuta uramu na utitiri mwingi wa rasilimali. Tunaparurana kwa harufu tu ya samaki. Hatujaona mnofu. Wasomi wetu hawajaandaliwa kupambana na ubeberu wa kimfumo katika mkutadha wa kimataifa, mfano ICC Kama taifa Hatujui kuwa tunaongozwa na itikadi gani; ya kijamaa au ya kibepari. Ni kizungumkuti! Ni mtikisiko wa kimaono. Kama tutasema tunajua tulikotoka na tulipo, lakini ni hakika hatujui tuendako. Msemo wa hayati Kolimba kama Taifa tumekosa dira. Abusolomo Kibanda anadakia akisema huko tuendako kweli  tutafika?  Ni mtaala ndio unaoweza kujibu haya yote.
 
Kwa maana nyingine kitendo cha kufuta matokeo ili kujipatia matoke mapya ya kupikwa ni sawa na kula chungwa lililooza ndani ya chumba kilichogubikwa na giza totoro huku tukijifariji kuwa, kwa vile hatuwaoni funza basi machungwa hayo hayana mathari kwetu. Hapa kama taifa, hatujajitendea haki hata kidogo. Tumejikaanga kwa mafuta yetu wenyewe!

Joshua Lawrence  0717047907

0 comments:

Post a Comment

SOCIAL NETWORKS

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

SEARCH IN THIS BLOG

JOIN ME ON FACEBOOK

BLOG FOLLOWERS

BLOG ACHIEVES

ADVERTISEMENT

ADVERTISEMENT

POPULAR NEWS

Je mtandao huu umekusaidia kujifunza na kupata maarifa Mapya...?