
Rais wa Senegal, Macky Sall akimkaribisha Rais wa Marekani, Barack Obama
katika Ikulu ya Dakar, Alhamisi iliyopita. Kushoto ni mke wa Obama,
Michelle. Picha na AFP.
Sera ya Mpango wa Rais wa Kupambana na
Malaria na HIV/AIDS (PEPFAR) ulibuniwa wakati wa Rais George W Bush na
umeendelea kwa misingi hiyo wakati wa Rais Obama na ziara yake hii
italenga zaidi eneo hilo.
Ujio wa Rais Barack Obama barani Afrika kwa mara
ya pili, na safari hii akikaa barani humu kwa takriban wiki moja, ni
hatua inayongojewa kwa shauku kubwa, lakini ambayo wafuatiliaji wa
habari na wataalamu wa uhusiano kati ya Afrika na Marekani wanashindwa
kusema nini hasa cha kutegemea.
Tofauti na ziara ya Rais Xi Jinping wa China hivi
karibuni, tena aliyofanya akianza kuingia madarakani - ya kwanza duniani
kuacha safari tangulizi ya Russia, ‘mtalaka’ wa China katika sera za
Kikomunisti za karne iliyopiga, ziara ya Obama haina matazamio ya miradi
mikubwa ya ujenzi, uwekezaji au vinginevyo. Ni wazi Afrika ni muhimu
zaidi kwa China hivi sasa kuliko ilivyo kwa Marekani na itabaki hivyo.
Wanaofuatilia takwimu za biashara wanasema kuwa
China imeshaipiku Marekani na nchi za Ulaya kama mshirika mkuu wa
biashara na Afrika, ila Ulaya ikiungwa pamoja kama Umoja wa Ulaya (EU)
bado ina biashara kubwa zaidi na Afrika kuliko China.
Marekani kwa maana hiyo ni ya tatu, lakini ni ya
pili kwa nchi moja moja, ingawa umuhimu wake kwa nchi za Afrika una
mapana zaidi ya jinsi hizo takwimu zinavyoonyesha.
Nchi hiyo ina hisa takriban asilimia 25 ya vyombo
vya fedha vya kimataifa, hasa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la
Kimataifa, kwa hiyo uhusiano wake na Afrika kwa sehemu kubwa unakwenda
kimya kimya, kama sehemu ya kazi za taasisi za kimataifa, si moja kwa
moja kama uhusiano
bayana.
bayana.
Ukilinganisha na China, tofauti kubwa kati ya
Marekani na China kwa Afrika na ndiyo tofauti inayoonekana katika ziara
za viongozi wakuu wa nchi hizo barani Afrika, ni kuwa uhusiano na China
ni wa kimkataba na biashara ya ana kwa ana. Uhusiano na Marekani una
mizizi katika mifumo ya biashara iliyopo duniani na sera zake
zinajulikana, hivyo unaweza kusoma mapitio na majadiliano kadhaa kuhusu
ujio wa Rais Obama barani Afrika usione chochote kuhusu uhusiano huo.
Sababu ni kuwa hayaamuliwi katika ziara kama hizi, ila ni sehemu ya
usawiri-mifumo ya biashara kimataifa, mielekeo ya kisera inayofuatiliwa
na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) na mifumo ya kudumu inayokubaliwa
na Bunge la Marekani.
Wakati kinachotajwa ni mikopo ya China kwa ajili
ya ujenzi wa miundombinu, ni rahisi kusahau kuwa mwelekeo wa kukuza
uchumi kwa mauzo ya nje kumeinuliwa sana na sheria ya Marekani ya AGOA
(African Growth and Opportunity Act) ambayo kwa miaka 10 sasa imekuwa
ufunguo wa nchi kuingia katika soko hilo. Tofauti kati ya nchi imetokana
na viwango vya ufanisi ndani ya nchi husika, na hapo ndipo
zinapoonekana tofauti kati ya wale wanaotazamia mengi sana kwa ujio wa
Rais Obama, na wale wanaotumia mifumo iliyopo ya biashara na Marekani.
Kwa mfano, Kenya inauza mara kumi au zaidi katika
soko hilo ukilinganisha na Tanzania, ila ziara ya Obama ni kwa Tanzania
na siyo Kenya; yupi mshirika halisi?
Mwelekeo wa Marekani katika biashara na Afrika
unatofautiana na China kimsingi kwa sababu Marekani imejikita katika
kuboresha uwezo wa Afrika kufanya biashara na kuvuta mitaji, ambayo
itaboresha uwezo wa uzalishaji, ufanisi katika sekta tofauti, na upana
zaidi wa sayansi na teknolojia. Marekani haitofautiani na Ulaya katika
suala hilo ingawa Ulaya imechukua muda kuoanisha ushirikiano na Afrika
katika mifumo ya kimataifa ya biashara kwa jumla, wakati Marekani ndiye
mlinzi halisi wa mifumo hiyo.
Hivyo Umoja wa Ulaya unachukua muongo mmoja
kujadiliana na Afrika nini cha kufanya baada ya uhusiano maalumu ya
mkataba wa Lome kuanzia mwaka 1973 yalipoisha kwa shinikizo la Marekani
mwaka 2007.
Marekani kwa upande wake haina muda wa kufanya
milolongo ya mijadala na nchi za Afrika kupambanua sera zake, bali
inaunda sera ndani ya michakato ya sera za vyama vya Republican na
Democratic, na kwa jumla ikishaundwa sera inakuwa ya kitaifa,
haibadiliki Serikali ya chama kingine ikiingia madarakani.
Kwa mfano, sera ya AGOA ilibuniwa wakati wa Rais Bill Clinton
kabla ya George W. Bush kuingia madarakani mwaka 2001 mwanzoni, na
haikubadilishwa lolote wakati wa utawala huo.
Kwa upande wa pili, sera ya Mpango wa Rais wa
Kupambana na Malaria na HIV/AIDS (PEPFAR) ulibuniwa wakati wa Rais Bush
na umeendelea kwa misingi hiyo wakati wa Rais Obama, na ziara yake hii
italenga zaidi eneo hilo.
Kabla ya Obama kuingia madarakani, kwa kipindi
kirefu hasa baada ya Afrika kufutiwa baadhi ya madeni yake na mengine
kuingizwa katika programu za malengo ya maendeleo ya milenia, watalamu
wa Afrika (kupitia mashirika tofauti ya kimataifa) walikuwa wanalilia
‘Marshall Plan’ ya Afrika. Ni mpango ambao aliyekuwa Waziri wa Mambo ya
Nje wa Marekani, George C. Marshall, aliyekuwa mmoja wa majenerali wake
wakuu wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, alibuni kuhusiana na Ulaya.
Afrika imelilia mpango kama huo ikidhania kuwa suala hapo ni fedha tu.
Dhana kuwa mpango kabambe wa kusaidia maendeleo ya
Afrika utawezesha kulivusha bara hilo kutoka umaskini na maisha ya
vijijini kuingia katika viwanda na maisha ya mijini ni potofu. Ndivyo,
pamoja na kuwa hapajawahi kuwepo mpango wa mara moja wa dola bilioni 500
labda kwa dola za sasa (walivyokuwa wakisema wataalamu wa Afrika miaka
10 au 15 iliyopita).
Takwimu za Marekani za mwaka 1947 zinaonyesha
kuwa wakati mpango huo unabuniwa, nchi hiyo ilikuwa na uzalishaji wa
jumla wa thamani ya dola bilioni 258, na ilitoa dola bilioni 13 baada
ya vita kumalizika, na dola bilioni 13 nyingine kwa ajili ya misaada ya
kiuchumi na kiufundi, kama sehemu ya mpango huo wa Marshall. Haikuwa ni
suala la kuijaza Ulaya kifedha; vizuizi vya biashara viliondolewa na
kuweka msingi wa kile ambacho baadaye kiliitwa Soko la Pamoja la Ulaya
na mwishowe Umoja wa Ulaya, kuweka misingi ya amani, utawala bora na
maendeleo bara lote.
Kimsingi, hii ndiyo sera iliyotumika kote duniani
kuinua nchi tofauti kutoka katika majivu na magofu ya Vita Kuu ya Pili
na mifarakani mingine iliyofuata, kuingia katika maendeleo endelevu
ambayo hayafuatwi na mikasa au milipuko ya kisiasa ndani ya nchi.
Wakati nchi za Afrika zinaelekea kufikia uhuru
mwelekeo wao wa fikra haukuwa na mpangilio huo, kwani ziliungwa mkono na
nchi za kijamaa, au za kikomunisti dhidi ya wakoloni, hivyo wakajenga
hisia kuwa Ulaya na Marekani zina nia ya kuwadhulumu, na kuwatawala
ikiwezekana. Hisia hiyo ilioana vyema na matakwa ya tabaka tawala baada
ya uhuru lililokuwa na nia ya kuzuia mali kuingia mikono ya wageni kwa
njia ya utandawazi (uhuru wa kununua hisa za makampuni, na kutokuwapo
sekta kubwa inayomilikiwa na serikali katika nyanja tofauti za uchumi,
n.k.) Ni sababu maendeleo kutokuwa endelevu Afrika.







0 comments:
Post a Comment