PAPA BENEDICT XVI, CHAMPIONI WAMABADILIKO

Saturday, July 6, 2013


Papa Benedict XVI amejiuzulu. Sasa anaitwa Papa Emeritus Benedict XVI. Ni Papa bado, lakini si kwa muktadha wa kiutawala ndani ya viunga vya  kanisa la Mtakatifu Petro pale Vatikano. Kwa maana nyingine hana nafasi ya kimaamuzi kuhusu mwelekeo wa kanisa Katoliki Ulimwenguni.

Kwa vile katika wadhifa huu wa juu kiuongozi, hakuna kustaafu, twaweza kuwa sahihi zaidi kama tukisema kuwa Papa huyu amepumzika milele huku akimwachia Papa mpya wa mabadiliko Francis I, ili aweze kuhitimisha ngwe muhimu ya mabadiliko katika muktadha wa Omega.

Hili ni tukio kubwa sana ambalo ni nadra sana kutokea, na kwa  kuzingatia u-nadra huo ni vigumu tukio hilo, kuzoeleka  kiasi cha kulifanya lipoteze alama za nyayo zake katika mchanga wa historia ya sayari hii, dunia.

Ndio maana ulimwengu wote, kwa muda, umelazimika kupitia  ndani ya mawimbi ya bahari ya mtikisiko uliotokana na mtibuko uliosababishwa na tukio hilo. Kwa hikika mawimbi ya habari ya tukio hilo kuu yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutengeneza mwelekeo mpya wa kufikiri juu ya hatima ya dunia. Wakazi wengi wa dunia wanajiuliza kwamba; Je, Papa huyu mpya toka Province ya Argentina ana nini kibindoni kwa ajili ya dunia inayosusulika kiuchumi kisiasa na kimaadili?

Wakati huo-huo, baadhi ya wafuatiliaji wa karibu wa mchakato huu ambao hadi sasa tayari umeshazaa mipasuko ya ki-mtazamo na ki-maoni kuhusu kiini cha kujiuzulu kwake, wanaitafsiri sababu ya kujiuzulu huko ndani ya muktadha wa ombwe la kiutawala; kwamba Benedict ameshindwa kuhimili vishindo vya mikiki-mikiki ya changamoto za kiutawala kutokana na umri wake kumtupa mkono, na hivyo. Kama Papa mdhofu amejikuta akiishiwa na maono na weledi wa namna ya kuliendesha kanisa katoliki katika nyayo zenye mikito sahihi ya kimaamuzi.

Shadidisho la mlengo huo wa kimtazamo ni kauli iliyobubujika kutoka kinywani mwa muhusika mwenyewe; kwani aliweka wazi sababu iliyomsukumu kufanya uamuzi huo mzito. Kama mwanadamu nimepungukiwa nguvu kimwili na kiakili kuweza kumudu changamoto za kuliongoza kanisa wakati huu. Ni maneno yake mwenyewe hayo. Hakuyamung’nya wala hakuyatafuna.

Wako wanaotegemeza mikito yao ya ki-msimamo ndani ya muktadha huo-huo; lakini wakiongezea minofu na rojorojo za kimantiki kwa mbali ili kukikoleza kiini cha kujiuzulu kwake. Hawa, wanamchora Papa Emeritus katika taswira ya kiongozi shujaa na mbobevu ndani ya ulingo wa kitheolojia na  kidogma- mhafidhina, lakini, aliyeshindwa kumaliza mbio zake kwa ushindi mnono baada ya kuishiwa pumzi.

Kimsingi, wachunguzi wa kada hii wanajaribu kumchora Papa Emeritus kama kiongozi dhaifu kiutendaji, aliyeshindwa kuyasimamia maono yake mapevu na yenye ushawishi mkubwa. Naam, maono yaliyoisukuma koleji ya  makadinali kumweka kwenye kiti cha enzi pale Vatikano dhidi ya mpinzani wake wa karibu kadinali Bergoglio kwenye Conclave ya mwaka 2005.

Wadadavuzi wa kada hii hawaoni mwanga ng’ambo ya ushahidi uliopo wa mituhumiano ya kashifa, mdororo wa maadili,kutetereka kwa hali za kiroho ya waumini na skandali mbalimbali ndani na nje ya viunga vya Vatikano vilivyomjengea Papa Emeritus taswira ‘fifi’ ya Papa mshindwa, kwamba vikichunguzwa kwa tafakuri jadidi vyaweza kuwa kete ya kumjengea Papa huyu taswira mpya na ng’avu;  taswira itakayomweka ndani ya wingu la machampioni, kama mmoja wa mashujaa wa ki-mikakati aliyefanikiwa kulisimamia, kuliongoza na kulijenga kanisa katika ramani  tukuka ya ki-jesuiti. Naam, na hivyo kustahili pumziko la amani akimwachia kijiti Papa wa utaratibu Mpya wa Dunia, Francis I ili aweze kumalizia ngwe muhimu ya kuuleta ulimwengu pamoja.

Kwa kuzingatia ibuko, yaani, dokezo ng’ambo ya muktadha huo mfinyu wa taswira fifi ya Papa Emeritus, akili ya kawaida inashawishika kuzama ndani, vilindini, si kwa kubeza kauli yake binafsi aliyoitoa juu ya sababu ya kujiuzulu kwake. Kwa namna yoyote ile. Kauli hiyo yenye kuibua mitafunano ya hoja ilikuwa na munyu wenye ladha ya hekima. Kwani angetoa kauli gani kwenye muktadha kama huo bila kuibua minong’ono na mitafunano ya kalamu za waandishi mahili?

Labda niseme kuwa, kwa mujibu kauli zenye kuiweka wazi hekima ya makadinali, uteuzi wa mapapa wenye umri mkubwa ni mbinu ya kimikakati inayowasaidia wateuliwa kufanya mambo kwa kasi zaidi. Huepuka kutengeneza mazingira ya mbweteko wa mapapa ndani ya curia kutokana na mtaji wa umri, hivyo hulazimika kumbizana na umri wao.

Kwa maana nyingine, hata uteuzi wa Papa huyu mwenye damu ya kirumi toka Argentina, Francis, ambaye hadi sasa  umri wake ni  miaka 76 akimzidi mtangulizi wake kwa miaka miwili ya  kipindi cha uteuzi wake mwaka 2005, ni strateji ile-ile ya kuhakikisha kuwa jesuiti huyu naleta mtikisiko wa dunia; Na tayari Tumeanza kuona cheche zake.

Niseme kwamba, kama ilivyo kawaida ya binadamu aliyejizoeza kuzifikirisha akili zake, asiyepalilia na kurutubisha fikra bweteko, mweleke wa kifikra wenye kumtafsiri Papa Emeritus kama kiongozi mshindwa- mdhofu wa mwili na akili hauzimi kabisa kiu au muwashawasha wa kuzama ndani kabisa ya viunga vya Vatikano ili kuibuka na taswira mbadala, pengine, isiyo na ukungu, ili kuangaza juu ya muktadha halisi wa kujiuzulu kwake.


Kwa jinsi mwenendo wa mambo ulivyo; Je, ni sahihi kuamini kuwa, Papa Emeritus Benedict ameamua kuchukua uamuzi mzito wa kujiuzulu kutokana, eti, na kuzidiwa na presha za kiutawala zisizoshabihiana na uwezo wake dhofu unaotokana na umri mkubwa? Je, sababu hiyo haijengi ushawishi mwingine akilini mwetu ya kuwa, kama ukweli ni huo, basi mapapa walioshindwa kujiuzulu japo walionekana kuwa na umri mkubwa na hata kudhofu kuliko Papa huyu walikuwa ving’ang’anizi wa madaraka? Mfano mzuri ni wa Papa Yohane Paulo II.

Hata hivyo, ukweli wa ziada ni huu: Upapa ni taasisi kubwa yenye kusimamiwa kikamilifu.  Si taasisi ya mtu binafsi hii. Maamuzi yoyote yale hufanyika kitaasisi kwa maslahi ya taasisi. Wakati Papa huyu akidai kuwa uwezo wake kiakili umedhofu, tayari amefanikiwa kuandika kitabu chenye kuibua changamoto kwenye ukanda wa kitheolojia kiitwacho “Jesus of Nazareth” kwa Kiswahili Yesu wa Nazareti, na yasemekana kuwa ana mpango wa kuandika kitabu kingine kitakachojikiti katika hoja tata kuhusu dhambi ya siri.

 Kuhusu kitabu hiki, “Jesus of Nazareth,” chenye kutoa mwangwi unaotoa sauti hafifu kwenye ukanda tulivu wa kitheolojia ya kuwa nguli huyu bado akingali na akili zinazoweza kusababisha mtibuko wa mawimbi ya bahari kwenye ukanda huu iwapo ataachwa huru, ni ushahidi mwingine ya kuwa Papa Emeritus si mdhofu. Na pengine ndiyo sababu atapaswa kujitenga na michakato ya ki-utendaji ili kuepuka migongano na hata misuguano isiyokuwa ya lazima. 

Narudia kusisitiza ya kuwa, huu ni ushahidi mnono ya kuwa bado akili zake zikingali na nguvu za kutengeneza mawimbi na hata mipasuko ya hapa na pale kitheolojia. Je,  kama ni hivyo angeshindwaje kulisimamia kanisa? Ana akili huyu. Upeo wake wa kufikiri bado una nguvu za ki-mitetemo inayoweza kulipeleka kanisa vileleni mwa ndelemo za ushindi! Kuamini kuwa mtu huyu ni mchofu mdhaifu kimwili, asiye na misuli ya kuweza kusimamia mwelekeo wa kanisa katika safari yake kuelekea vileleni mwa ushindi, ni sawa na kupalilia wazo jingine chovu tete na dhaifu ya kuwa Upapa unahitaji mtu mwenye misuli  na nguvu za kubeba zege au vitu vizito.

Kwa maana nyingine tukio la kujiuzulu kwa Papa Emeritus haliwezi kuwa ni la kushitukiza, kama ilivyotafsirika kwa wale walio nje ya mduara wa kimaamuzi. Hii ni nafasi nyeti yenye kusimamiwa kwa kuzingatia unyeti huo-huo. Tukio hili halikuwa na kamwe haliwezi kuwa la kushitukiza, na, ni lazima lilipangwa ki-mikakati chini ya usimamizi wa mainjinia wenye akili pevu. Kwanini? Kwa sababu hata kama sababu ya uzee ingekuwa na mashiko, uzee hauji kwa siku moja, ni suala la ki-mchakato pia! Kwani daktari wake, na hata washauri wake wa karibu walikuwa wapi hadi kupelekea Papa Emeritus afikio uamuzi kujiuzulu, tunaoambiwa kuwa, eti, ni wa kushitukiza?

Kuamini kuwa uamuzi wa Papa Emeritus ulikuwa ni wa kushitukiza, na, ulitokana na utashi wake binafsi baada ya kujipima na kujiona kuwa hawezi kumudu nafasi hiyo, waweza kukubalika tu kama ganda la nje linalofunika ukweli “kiini” wa kujiuzulu kwake. Ni utetezi unaoweza kupewa uzito sitahiki, kwa muktadha, tu, wa kuutathimini upapa kama kitengo cha mtu binafsi, na wala siyo taasisi mbuyu kupita zote duniani. Na hapo ndipo sauti zinasikika zikiuliza kwa hamu juu ya hicho kiitwacho ukweli kiini,  Ni upi ukweli huo? Subiri tutaona mbele ya safari.

Na hata hivyo, kukubaliana na utetezi huo kama ndiyo sababu pekee ya kujiuzulu kwake ni sawa na kutilia wasiwasi hekima ya koleji ya makadinali, iliyotumika kumchagua Papa huyu mnamo mwaka 2005; kwani kabla na hata baada ya uchaguzi kufanyika wadadisi  wengi walitilia shaka umri wake kwamba ulikuwa tayari umemtupa mkono, lakini Conclave ilitathimini haya yote na kuona ni hekima na busara kumweka Papa Emeritus kitini pa Enzi.

Kwa vile jopo la makadinali lililompitisha Papa huyu lilisheheni wana-mikakati wazoefu- wasomi wabobevu wanaotambua ndani na nje ya unyeti wa nafasi ya Upapa kama taasisi mbuyu, ni uvivu wa kufikiri utakaotufanya tunyamazishwe na hicho tulichopewa, ambacho kwa hakika hakishibishi akili tunduizi; ni sahihi zaidi kama tutatafuta nguzo nyingine imara ya kutegemeza imani zetu.

Katika hili, wapo watu wanaohoji hata sababu ya mivumo na mivujo ya skandali iliyomchora Papa huyo aonekane kuwa ameshindwa kulisimamia kanisa vizuri, kuibukia zaidi ndani ya mwaka 2012 na hivyo kuutia mhuri uhalali wa hatua yake ya kujiuzulu aliyoichukua mwanzoni mwa mwaka 2013. Je, hiyo haikuwa mipango ratibivu ya ki-jesuiti inayoendana na ajenda ya utaratibu mpya wa dunia unaopaswa kuanza mwanzoni mwa mwaka 2013? Wadadisi wanahoji.

Wanaenda mbali zaidi, wakihoji pia, hata, sababu ya kadinali mwenye kupewa heshima kubwa kutoa taarifa mwanzoni mwa mwaka 2012 ya kuwa  kuna njama zinazoendelea chini kwa chini ili kumwangamiza Papa Emeritus kabla ya Oktoba!

Pamoja na ukweli kuwa Msemaji wa Vatikani hakusigana na uwepo wa taarifa hiyo, zaidi ya kutokubaliana na ukweli wa tetesi hizo, bado uwepo tu wa tetesi hizo ulikuwa tayari umefinyanga wazo la uhalali wa ung’atufu wake ndani ya mwaka 2013. 

Twaweza kupata hitimisho safi, si kwa namna ya kutumia staili ya kupapasa na kudodosa-dodosa mambo, bali ni kwa jambo moja: kuwa na picha kamili ya uwezo, vipaji lukuki, maono na hata  utendaji wa Papa Emeritus kabla ya kushika wadhifa huu mkubwa wa Upapa.

Kabla ya kutunukiwa wadhifa huo, akiwa kadinali kwa jina la Joseph Ratzinger, aliteuliwa na Papa Yohane Paulo II kusimamia kitengo nyeti cha mafundisho ya kanisa katoliki ulimwengu, kitengo ambacho hivi sasa kinashikiliwa na kadinali toka nchi ya Ghana-kadinali Peter Turkson.

Utendaji wake kwenye kitengo hiki nyeti, bila shaka yoyote, ulikuwa ni wa kiwango cha juu. Usio na kasoro; japo baadhi ya wahafidhina ndani ya taasisi hii, kwa kushindwa kumweka ndani; yaani, katikati kabisa ya viganja vya akili zao za ki-mtazamo, naamini kuwa ni kutokana na kuzidiwa na upeo wake wa kimaono juu ya namna ambavyo taasisi hii mbuyu inavyopaswa kuendeshwa ili iweze kuutwaa ufalme wa dunia hii mwanzoni mwa  mileni ya tatu,  walimwona kama kiongozi mwasi anayetaka kulipeleka kanisa ndiko siko.

Misimamo yake ya kiliberali na vikolezo vyenye ladha ya kihafidhina kwa mbali, kama alivyosomeka na kutafsirika, viliwachanganya watafiti na hata wachunguzi wa juu-juu walio ndani na nje ya taasisi hii. Na hivi ndivyo baadhi yao wameendelea kuchanganywa na msimamo usiotabirika wa Papa huyu mpya toka jamii ya ki-jesuiti toka Agentina hata kabla ya kushika wadhifa huo.

Kama ushahidi wa hili, miaka minane iliyopita kabla tu ya Conclave ya mwisho iliyomteua Papa Emeritus, msemaji wa  jamii ya Ki-jesuiti Jose Mana de Vera alimpambanua kadinali  Jorge Mario Bergoglio, kabla ya kuvishwa kofia ya Upapa kama kadinali wa ki-jesuiti asiyeweza kupewa asilimia zote 100 kama jesuiti kamili; pia aliwahi kumwambia mwandishi  mashuhuri wa ki-Agerntina, Sebastian Lacunza ya kwamba kadinali huyu anaonekana kuvutia na baadhi tu ya mambo ya ki-jesuiti.

Kwa sababu ya kujichorea taswira hiyo, yenye ukungu-ukungu kwa mbali, baadhi ya wadadavuzi wanahoji, pia, hata sababu iliyompelekea kufanya uamuzi wa kujipa jina la Francis wa Asisis badala ya jina la Francis Xavier, jina la  aliyekuwa jesuiti, na mwasisi mwenza wa jamii hii inaloendesha mambo yake nyuma ya pazia la Vatikano, akishirikiana na Iginatus Loyola. Jambo la ajabu ni kuwa hawa wote wana jina moja la Francis! Je, hatuwezi kutegemea haiba za watu hawa wawili zikikumbatiana na kubusiana  ndani ya Papa Francis?

Iwapo, wanajiuliza, Papa huyu anaonekana  kutofungamana na mwenendo wa ujesuiti, japo si kweli, aliwezaje kupenya ngome ya ki-Conclave, ambayo ni nadra sana kwa kadinali anayesigana na maono ya ki-jesuiti kuweza kupenya?

Je, itakuwa sahihi kuamini kwamba makadinali hawa wamemchagua kadinali toka shirika la ki-jesuiti mwenye msimamo utakaoleta misigano dhidi ya maono ya ki-jesuiti, ambayo kimsingi ndiyo yanayoliongoza kanisa hili kuelekea vileleni mwa ushindi ? Kumekuwa na migongano ya hapa na pale iliyokuwa ikitengeneza misuguano baina ya mwenendo wa ki-jesuiti.

Je, kwa vile Papa Francis ndiye Papa wa kwanza toka jamii hii ya kijesuiti inayotenda mambo yake nyuma ya pazia; na kwa vile lengo kuu la majesuiti ni kuhakikisha kuwa wanatawala hazina zote za dunia pamoja na mifumo yote ya kiutawala, twawezaje kupingana na hoja za kikadinali zenye kuleta mategemeo chanya kwa kanisa Katoliki kuwa Papa Francis ndiye kiongozi wa matengenezo atakayelipa kanisa sura sitahiki?

Na; Je, uvumi unaoenezwa na vyombo vya habari, ukiwanukuu makadinali wanaodai kuwa, eti, Papa Francis hakufahamika sana, na kwamba hakutegemewa kuchukua wadhifa huo mzito una nguvu? Iwapo uwezo wake wa kulisimamia kanisa huko Latin Amerika dhidi ya mvuto wa makanisa ya kiprotestanti yakiwemo yale ya kipentekoste  umeweza kumpa karata turufu ya kushika wadhifa huo, inahitajika akili iliyodhofu kukubaliana na uvumi huo wenye harufu ya ki-propoganda.

Naam, huo ni uvumi  wenye mguso dhaifu usioweza  kuingia akilini  mwa mtu mwenye tafakuri jadidi; ukizingatia kuwa Papa Francis I alikuwa ndiye mshindani wa karibu wa papa mjiuzulu, Benedict. Kwa maana nyingine jopo la makadinali walioshiriki Conclave ya mwaka 2005 na hata waliokuja kuteuliwa na Papa Benedict wakati akiwa kiongozi wa kanisa pale Vatikano walikuwa wameguswa na cheche zake, na kwa hakika hawa wote walikuwa na fursa adhimu ya kuupima uwezo na maono yake mapevu ya ki-jesuiti, kama kadinali mwenye sifa za kuwa Papa mtarajiwa.

Tukio la Kadinali Bergoglio, hatimaye, kuchagulia kushika wadhifa huu nyeti katika wakati ambapo dunia inapaswa kuwa moja ni ushahidi usioweza kutiliwa mashaka ya kuwa Papa Francis I amefanikiwa kuketi kwenye kiti cha enzi kama  matokeo ya koleji ya makadinali wa Conclave hiyo kuchezesha karata zao sawasawa, wakiamini kuwa huyu ndiye Papa muhimu kwa wakati muhimu wa historia ya mabadiliko ya sayari hii. Kwa nini? Sura ya tatu ya kitabu hiki ina majibu toshelezi kwa kila mwenye jicho dadisi kwa swali hili jadidi.

Kabla ya kuhitimisha safari yetu inayompembua Papa Emeritus kama championi ndani ya wigo wa ki-mikakati kuelekea serikali moja ya dunia, ni vema tukapitia baadhi ya misimamo ya ki-theolojia ya Papa huyu  iliyomtengenezea taswira “fifi”  ya ukengeufu.

Hata hivyo taswira hiyo, si tu kwamba, yaweza kuwa ndiyo karata yake iliyompa turufu ya kukitwaa kiti cha enzi baada ya kufariki kwa Papa Yohane Paulo, bali pia waweza kuwa ushahidi mpevu ya kuwa Papa Benedict, wakati huo akiwa kadinali Joseph Ratzinger, alikuwa ndiye nguvu nyuma ya mafanikio ya hayati Papa Yohane Paulo II.

Ni Papa huyu,  Yohane, ambaye historia imeona aibu kuuficha ukweli uhusuo utendaji wake mtukuka ndani ya kifusi cha masalio, kama propaganda za mpito, ya kuwa  katika kipindi cha utawala wake, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuliweka kanisa Katoliki kwenye ramani ya dunia kama taasisi yenye maghala ya raslimali watu, ukwesi usiomithilika na mtandao mpana wenye uwezo wa kufanikisha mpango wa kuinjinia serikali moja ya dunia.

Kwa namna nyingine, ni vigumu kumtenga Papa Emeritus na mafanikio ya ki-Ekumene, ki-diplomasia na hata ya ki-haiba ya nafasi ya Upapa yaliyopatikana ndani ya kipindi  kirefu cha Papa Yohane Paulo II. Kwani akiwa kama injinia wa kitheolojia kwenye kitengo cha mafundisho ya kanisa kwa kimombo ‘The Congregation for the Doctrine of Faith’ alikua na mchango mkubwa katika  kulitengenezea kanisa haiba yenye mvuto; haiba iliyotakata, japo si kwa kiwango kitakacholetwa na Papa huyu wa New world order, haiba yenye rangi inayokubalika ulimwenguni.

Akiwa kadinali mwenye kujipambanua kama msomi katika kiwango cha u-profesa - mwana-falsafa na mwana-theolojia asiyeweza kutiliwa shaka ndani ya ukanda wa kidogma, alikuwa chachu katika kuhakikisha kuwa msingi imara wa daraja la ki-ekumene  na kidiplomasia, kama nilivyogusia huko nyuma, unatengezwa. 

Profesa Malachi Martin ndani ya kitabu chake mashuhuri, The Keys of this Blood ukurasa wa 17 anatupa picha halisi ya maono makubwa ya Papa Yohane Paulo II yaliyokuwa kama injini inayoongoza usimamizi wa  sera kipaumbele kuelekea vileleni mwa ushindi. Anasema, “It is not too much to say, in fact, that the chosen purpose of John Paul’s pontificate- the engine that drives his papal grand policy and that determines his day to day, year-by-year strategies is to be the victor in that competition, now well under way” Kwamba “si kuzidisha chumvi  kusema, kwa hakika, kuwa kusudi teule la upapa wa Yohane Paulo- injini inayosukuma sera mtambuka na kile kinachoamua mikakati ya siku kwa siku na mwaka hadi mwaka ni kuwa mshindi kwenye kinyang’anyiro ambacho hivi sasa kinaendelea vizuri.”

Akiwa memba wa “The Committee of 300” familia zenye ushirikiano wa damu barani Ulaya, halikuwa jambo la ajabu kwa yeye kuwa muhimili muhimu katika kuhakikisha kuwa Ulaya, kama eneo rutubivu kwa ustawishaji wa mpango wa kuinjinia Utaratibu Mpya wa dunia linakuwa chini ya himaya ya Vatikano.

Profesa Martin akiichambua njozi ya Papa Yohane Paulo anasema, In John Paul’s geopolitical analysis, Europe from Baltic to the Adriatic Sea is the center of that power, the Holy Father’s battle was to control that center. Tafsiri. Kuhusu mtizamo wa kijiopolitiki wa Yohane Paulo  Ulaya toka Baltik hadi  Bahari ya Adriatic  ndiyo kitovu cha uwezo.  Vita vya Baba mtakatifu vilikuwa ni kukitawala kitovu hicho.

Ikumbukwe kuwa njozi na maono ya hayati Yohane Paulo havikuwa ubunifu wake mwenyewe, bali huo ulikuwa  ni mpango wenye mizizi ya ki-taasisi na wenye matawi toka ndani ya Ikulu ya Vatikano. Ni mpango wa kanisa Katoliki kama taasisi, kwa kushirikiana na wapambe wake wa karibu, huku ma-jesuiti wakiwa ndiyo watendaji wakuu nyuma ya mpango huo mpevu.

Ni mtazamo wa Vatikano wenye ladha tamu, lakini chachu  kitheolojia kwamba ujenzi wa Utaratibu Mpya wa Dunia bila Mungu ni sawa na maluweluwe; na kwamba taasisi hii chini ya Papa ndiyo yenye mamlaka ya kiungu kwa ajili ya kufanikisha mpango huo. Ijapokuwa mtazamo huo, kwa sehemu, una usahihi wake. bado unahitaji ukarabati ili usikinzane na Maandiko Matakatifu; kwani unatengeneza wazo jipwa, na tete, ki-theolojia linalosigana na Maandiko Matakatifu likitunong’oneza kuamini kwamba; “ni mpango wa Mungu kuanzishwa serikali moja ya dunia kupitia serikali hizi za wanadamu walioanguka dhambini, wakati ukweli ni kwamba Mungu hana mpango huo.”

Malachi anaandika hivi; Clearly  the new agenda-Heaven’s agenda; the Grand Design of God for the new world order- had begun. And Pope John Poul would stride now in the arena of the millennium endgame as something more than a geopolitical giant of his age. He was, and remains, the serene and confident servant of the Grand Design. Kwa uwazi bila kificho, Profesa Malachi Malachi Martin anaanika siri hii muhimu ya kuwa New world order ni ajenda kuu ya Mungu iliyo ya kimbingu  ikiwa mbioni kukamilishwa na Vatikano; na akiandika kuhusu mwanzo huo; anasema Yohane Paulo anajizatiti sasa kwenye kinyanganyiro hicho cha mwisho wa mchezo wa milenia kama jambo lililo kubwa zaidi ya mashindano makubwa ya kipindi chake ya kutawala siasa za dunia. Anahitimisha kwa kuandika kuwa Papa Yohane Paulo,  Alikuwa, na anadumu kuwa mtumishi mteule wa mpango huo mpevu.

 Yohane Paulo akiwa ziarani Czechoslovakia Aprili 1990 alitamka maneno haya; The claim to build a world without God has been shown to be an illusion… such a hope has already revealed itself as a tragic utopia… for man is unable to be happy if the transcendent relationship with God is excluded akiwa na maana kuwa dai la kuunda dunia isiyokuwa na Mungu limeonekana kuwa ni kujilisha upepo… tumaini kama hilo limejifunua lenyewe kama mkasa wa matumaini ya kufikirika… kwani mwanadamu hawezi kuwa na furaha kama uhusiano na Mungu umewekwa kando.

Mpango wa kuunda Utaratibu mpya wa dunia chini ya usimamizi na msukumo wa Vatikano, ni sehemu ya utimizo wa unabii wa nabii Danieli ya kwamba nyakati za mwisho kabla tu ya kurudi kwa Yesu mara ya pili kutakuwa na jitihada za dhati za kuifufua dola ya Rumi iliyosambaratika. Ki-msingi, kama hayati Yohane Paulo alivyowahi kutamka, jitihada za kuutawala ulimwengu ni lazima zianzie pale Ulaya- Rumi iliyosambaratika mnamo karne ya tano “Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.” Danieli 2:43

Na hata kile, naamini,  kinachodaiwa kuwa ni kushindwa kwa Papa huyu kulisimamia kanisa hili dhidi ya minyukano kashifa, mdororo wa maadili ndani na nje ya kanisa, kuvuja kwa nyaraka za siri, zikiwemo za kifreemasons, si jambo la kiajali, niseme, ni sehemu ya mchakato ndani ya muktadha mpana wa program inayohitaji uwekezaji wa misuli ya fikra pevu- The New World Order. Tutaona.

Kwa wale wasiojua maono na mtazamo wa awali wa Kadinali Joseph Ratzinger, kabla ya kushika wadhifa wa Upapa, waweza kushangazwa na habari hizi, kwamba, kadinali huyu aliwahi kumshauri Papa Yohane Paulo ili achukue hatua stahiki dhidi ya mdororo wa kimaadili mgawanyiko wa ki-mtazamo na matatizo mengine yaliyokuwa yakiliandama kanisa la Roma.
Malachi Martin kama mmoja wa wasiri wakuu wa michakato inayoendelea pale Vatikano anaandika kuwa The Pope turned on Ratzinger with a sharp and open rebuke of all kind rarely seen in the Apostolic palace, kwa Kiswahili ni kuwa Papa alimgeukia Ratzinger kwa kemeo kali na la wazi ambalo ni nadra kuonekana kwenye Ikulu ya kitume. Papa Yohane alikataa kabisa kutumia machafuko yaliyokuwa yakiliandama kanisa ili kutengeneza  utaratibu. “He refused to bring order out of chaos” Keys of this Blood uk 85

Kwa kuzingatia maono ya Papa Yohane Paulo, ambayo hatimaye yalikuja kuendelezwa na Papa Benedict, ilikuwa ni kuhakikisha kuwa kanisa linaepuka mwelekeo wa  kidogma unaokumbatia utamaduni   unalitambulisha kanisa katoliki kwa ulimwengu kama kanisa pekee la kweli la Kristo. Sababu kuu ni kuwa, kukumbatia utamaduni huo, ndani ya mchakato mpevu wa ki-ekumene kungelifanya kanisa liwe kisiwa na hivyo kushindwa kufanikisha mpango huo.

Ni uongofu na ubatizo ndani ya kisima cha maono hayo mapevu ndiyo uliyomsukuma kadinali Joseph Ratzinger kujifungia ndani ya vyumba vya Vatikano ili kuyatathimini baadhi ya mafundisho na misimamo ya ki-dogima na hatimaye kuikarabati ili iweze kuwa na sura ya ki-ekumene, kama tutakavyoipitia baadhi ya misimamo hiyo, kwenye sura ya tatu ya kitabu hiki.

 Kwa mantiki hiyo, jitihada zozote za kujaribu kumtenga Papa Emeritus Benedict na mafanikio ya hayati Papa Yohane Paulo II, ambapo hadi hivi sasa kama sehemu tu ya matunda ya jitihada hizo, tunashuhudia shirikisho la Ulaya likizinduliwa mwaka 2014, ni sawa na kujaribu kuishawishi dunia kuwa cheo cha Upapa ni sawa na kisiwa cha Patimo, eneo ambalo uwepo wa uhai wa binadamu unategemea  kudra tu.

0 comments:

Post a Comment

SOCIAL NETWORKS

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

SEARCH IN THIS BLOG

JOIN ME ON FACEBOOK

BLOG FOLLOWERS

BLOG ACHIEVES

ADVERTISEMENT

ADVERTISEMENT

POPULAR NEWS

Je mtandao huu umekusaidia kujifunza na kupata maarifa Mapya...?