RAIS OBAMA: NA PROPAGANDA ZA KUTAWALA FIKRA ZA WASOMI WA KIAFRIKA

Thursday, July 4, 2013




Uko mkakati mzito unaoendelea chini kwa chini ili kuhakikisha kuwa  dunia yote inatweka vilindini mwa  mfumo wa kimaadili unaopwaya  siku si mbali tokea sasa. Kwa hakika huo ni mkakati  yakinifu unaoratibiwa kwa weledi mkubwa huku watu wenye misuli ya kimaamuzi wakishikilia mwelekeo mzima wa  ajenda hii tete na tata; Tutaangalia.

Wakati msukumo huo ukiendelea kutengeneza mwelekeo wa kimaadili ulio legelege, huku wale wote wanaojitahidi kusimama katika misingi kimaadili wakiwekwa fungu moja na kundi ya wahafidhina, watu waliathiriwa na misimamo ya kidogima isiyofungua wigo kwa mawazo mapya, kuna kila dalili zinazoonesha kuwa hatimaye dunia nzima, isipokuwa kundi la watu wachache, itapigishwa magoti chini ya bendera ya mfumo  wa kimaadili mdhofu utakaokuwa kama jeneza la mataifa tayari kwa mazishi.

Hatari iliyo kubwa zaidi, ni pale  hoja hizi momonyovu kimaadili zinapopenyezwa taratibu ndani ya mifumo ya kisheria huku zikiwa zimevikwa magwandwa yenye rangi  ya kidemokrasia na usawa kwa wote na hivyo kulichora kundi kinzani katika taswira fifi iliosheheni makengeza ya hitifaki ya usasa, unaoenzi misingi ya usawa na utu!

Mkakati huo unakwenda sambamba na upropagandisha uliokubuhu kwa hila, ili kutengeneza taswira isiyo sahihi kuhusu muktadha jumla wa dhana nzima ya neno maendeleo. Kwamba, wakati muktadha  uhusuo dhana ya maendeleo ya kweli wapaswa kumulikwa katika nyanja zote kwa ukamilifu wake, yaani; kiakili, kiafya, kimaadili na matumizi sahihi ya raslimali ndani ya kijamii husika, mataifa ya magharibi yanajaribu kujikita zaidi katika mtazamo finyu wa utajiri wa vitu; nyumba, magari, na vikorombwezo vyake, huku maeneo mengine muhimu hata kuzidi vikorombwezo hivyo yakiacha pembeni.



Katika harakati zao za kuudororesha mfumo wa kimaadili, tarehe 17 Juni mwaka 2011 dunia yote ilishuhudi Umoja wa Mataifa ukipitisha ajenda ya kuhalalisha ndoa ya jinsia moja. Tamko hilo lenye ukakasi kimaadili,  ambalo kwa lugha sahihi nituseme ni azimio la umoja wa Mataifa, lilisomwa na aliyekuwa katibu wa Rais Barack Obama bibi Hilary Clinton. Afrika Kusini ndio Waliokuwa wafadhili wakuu wa michakato yote hadi hitimisho lake.

Baada tu ya tamko hilo, ulimwengu umeshuhudia anguko la ghafla kimaadili huku matamko toka vinywa vizito yakijitahidi kuinawilisha ajenda hii kwa lengo la kuijengea misuli  ya  kimvuto ndani ya katiba za nchi mbalimbali duniani. Mataifa yaliyoongeza msululu ndani ya safari ya mporomoko kimaadili ni kama vile  Uingereza, Ufaransa, na mengine yako mbioni kufuata foreni hii, inayoongozwa na mkuu wa giza!

Katika hili, Umoja wa Mataifa chini ya Katibu Mkuu wa sasa, mheshimiwa Ban ki Moon, umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa viongozi wa juu wa mataifa yote wanasimamia kwa umakini mkubwa  utekelezaji wa azimio hili; Tanzania ni moja ya nchi wahanga wa msukumo huo wenye ladha ya kisodoma na Gomora!

Ukiwa kama mwendelezo wa ajenda hii, hivi karibuni katika ziara yake barani Afrika, akiwa nchi Senegal, Barack Obama, ametoa hotuba mbele ya Rais wa nchi hiyo akihimiza kuwa yeye kama muumini wa usawa, angependa kuona kuwa mashoga wanapewa haki yao kisheria pasipo kubaguliwa. Hata hivyo kauli hiyo ilijibiwa hapo-hapo na Rais huyo jasiri akisema kuwa katu taifa lake haliwezi kusigana na maadili ya kitaifa kwa kuhalalisha ushenzi huo.

Hata hivyo jibu hilo lenye mshehenezo wa hekima ya kimbingu halikumfanya rais Obama kuendelea na kile ambacho kwa hakika kingeweza kutafsirika kama mashindano, ndani ya mdahalo usio rasmi, zaidi ya kumalizia kwa kusema kuwa yeye kama Rais wa Marekani mwenye kuamini juu ya usawa, hayupo pale kwa lengo la majadiliano.

Wadadavuzi wabobevu wa siasa za dunia, wanaamini kuwa kauli ya Obama yaweza kubeba uzito mkubwa kuliko ambao bongo zenye kunyanyapaa usumbufu wa kufikiri zinavyoweza kuipa.  Na, kwamba hakuna taifa lenye utapiamlo kimaadili liwezalo kusonga mbele kiuchumi. Historia imehifadhi kwa uaminifu kumbukumbu ya anguko la mataifa makubwa yaliyowahi kutikisa dunia ikiwemo dola ya Rumi, ya kwamba sababu ya anguko la mataifa haya yote ilitokana na kutindikiwa kimaadili kulikoyafanya yashindwe kujisimamia yenyewe.  

Kwa mwanga ulio bora zaidi, Obama hafanyi ziara Afrika kwa lengo ya kutafuta, tuseme, mwafaka wenye kutegemezwa na uhuru wa waafrika kujiamulia masuala yao ndani ya mataifa yao, bali ni sehemu ya mwendelezo wa mradi mpevu wa kuhandisi bongo za wasomi wetu katika mwelekeo utakaokuwa na tija kwa taifa la Marekani na wapambe wake, huku miundombinu ya kimaadili ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli ikiporomoshwa chini kupitia propaganda fifi zenye ladha feki ya upanuzi wa demokrasia.

Hata kongamano lililobeba jina tukufu “Global Smart Partnerships” si wazo handisivu kupitia vinu vya bongo za  waafrika, bali ni mwendelezo wa propaganda za kimagharibi zenye lengo la kuwapumbaza waafrika, ili waendelee kupigana na adui feki kiuchumi, ambaye kwa hakika siyo mvio wa mataifa ya Afrika kiteknolojia, bali ni mvio wa bongo za wasomi wetu, na tiba ya kweli yapaswa kujikita hapo.
Kwa hakika, jitihada zozote zisizojikita katika ujenzi wa miundombinu ya kimaadili na kimenejimenti ndani ya mkutadha wa ombwe la usimamizi makini wa rasilimali vitu na watu, hugeuka  sehemu ya mwendelezo wa usambaratishaji wa maadili, kwa maana ya kutoruhusu uwekevu wa mawazo mapevu juu ya adui wa kweli wa mataifa ya kiafrika, ambaye ni udhaifu wa kusimamia raslimali zilizopo, zikiwemo raslimali watu kwa ajili ya manufaa ya waafrika.

Udhaifu huo ndiyo uliofanikisha uundwaji wa dola za kifisadi zenye kutengeneza minyororo yenye miale mikali itiayo  kiwi mboni za wahandisi wenye uzalendo na bara hili ikiwemo Tanzania. Kwa mfano; ni nani asiyejua kwamba Symbion ni mjukuu wa Richmond aliyetuzalia watanzania mwana wa pekee kwa nina aitwaye Downs.

Je, intelijensia ya Barack Obama haijampa taarifa juu ya sakata hili. Ya kuwa joka linalokunya maziwa ya watanzania linafugwa na Amerika? Kama kweli Obama ana nia ya dhati ya kuwakomboa waafrika, na, anatutakia watanzania jioni njema yenye mafanikio kiuchumi; Kwanini  atumie wakati wake wa thamani kubariki ufisadi uliopo pale Ubungo badala ya kuusambaratisha kupitia mjadara wa kimataifa kama huo?

Kuhusu mada inayojenga dailojia ya “Global Smart Partnerships; Je, ni kweli kwamba tunahitaji teknolojia ya hali ya juu ili tuvuke hapa tulipo kiuchumi? Je, ili kubaini ukweli ya kwamba, wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya madini, wakiwemo wamarekani wenyewe hawalipi kodi na hivyo kulidumaza taifa kiuchumi kwa kulikosesha mapato ambayo ni muhimu kwa maendeleo kiuchumi, kweli tunahitaji teknolojia?

Je, tunahitaji teknolojia ili kubaini wizi wa mamilioni ya tani za minofu ya samaki yanayosafirishwa kwa meli kila siku kwenda china na penginepo? Nauliza watanzania wenzangu, naomba majibu stahiki! Je, ili kutambua kuwa utajiri wa uramu na gesi tulio nao waweza kututoa kutoka kwenye lindi la umaskini hadi kuwa vileleni mwa mataifa tajiri iwapo tutatanguliza uzalendo tunahitaji teknolojia gani?

Je, tunahitaji teknolojia ili kuzuia utoroshaji wa wanyama, na uvunaji wa magogo huku udongo wenye madini na vito vikisafirishwa kwenda ughaibuni kwa gia iliyojaa ghiliba?

Si kwamba napingana na uwekezaji kwenye Elimu ya teknoloji, bali siamini kwa Afrika iko nyuma kimaendeleo kwa sababu iko nyuma kiteknolojia. Hizo ni propaganda za mataifa ya magharibi Hoja mtambuka ni kwamba; kwa kusimamia  raslimali zetu kwa uadilifu huku tukitangukliza uzalendo tungefika mbali sana kiuchumi. Kuna mifano ya nchi za kiarabu ambazo kwa usimamizi wa mafuta tu, hivi sasa ni tajiri, mfano Botswana, kwa kusimamia vizuri madini ya dhahabu hali za wananchi wake ni bora.

 Mjadala wa Global Smart Partnerships ungetutendea haki waafrika kama ungelenga katika kupambana na mfumo kandamizi wa mataifa makubwa kupitia World Bank na IMF. Mjadala huo ingeleta tija kiuchumi kama ungelenga katika kuyabana makampuni ya kigeni yanayokwepa kodi na uwekezaji katika ardhi ya waafrika uliokosa rojo ya urari. Naam, mjadala huo ungejielekeza katika kuwabana watawala, na sio viongozi, wa kiafrika wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kukandamiza demokrasia yenye mshehenezo wa maadili safi yanayokinzana na demokrasi ya kuruhusu ushoga.

Bara la Afrika haliwezi kutegemea ukombozi wa kweli kiuchumi kupitia mawazo na makongamano yaliyohandisiwa kwa weledi mkubwa na mataifa ya magharibi. Huko ni kujidanganya, kwani roho ya kutawala fikra za waafrika iliyowatafuna mababu zetu nyakati za ukoloni mkongwe  ni ileile inayojipambambanua katika sura ya utandawazi.

Kwa jinsi mwelekeo wa mambo ulivyo ni vema nikahitimisha makala hii kwa kutamka bayana kuwa, ili kujikomboa kiuchumi, Afrika inahitaji Afrika Smart Partnerships na siyo Global Smart Partnerships.
Kuendelea kukumbatia fikra za kizungu kama nyenzo ya kututoa hapa tulipo,  hakutofautiani kabisa na ukahaba wa akili unaokwenda sambamba na ukuadishaji wa bongo za kisomi ndani ya mzunguko usio na mwisho wa fikra mfilisi zinazotegemezwa na mirindimo ya fikra twezo za kimagharibi. Tafakari  kasha chukua hatua!

drjoshualawrence@yahoo.com au 0753333003



0 comments:

Post a Comment

SOCIAL NETWORKS

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

SEARCH IN THIS BLOG

JOIN ME ON FACEBOOK

BLOG FOLLOWERS

BLOG ACHIEVES

ADVERTISEMENT

ADVERTISEMENT

POPULAR NEWS

Je mtandao huu umekusaidia kujifunza na kupata maarifa Mapya...?